UKUMBUSHO WA MAREHEMU GEORGE OMOYI LUKOBAGeorge Omoyi alizaliwa mwaka 1937 katika Kijiji cha Ebuloma, katika lokesheni ndogo ya Nasira, Bukhayo, Wilaya ya Busia. Alikuwa mtoto wa kwanza wa marehemu Mzee Ibrahim Lukoba Odulwa na Mama Monica Christine Auma Lukoba (Namani).
‘Omoyi’ ndio jina alilopewa ya Kiteso kwa heshima ya mchunga wanyama mwaminifu kabisa aliye saidia wakati alipo kuwa akizaliwa. Akiwa mtoto, nyanyake marehemu mpendwa Munyakho (Nakhabi), alisaidia kumlea, nyanyake alimpenda sana marehemu na alimfunza mengi kumtayarisha kwa maisha ya mbeleni ikiwa ni pamoja na jinsi ya kusiaga unga akitumia mawe ya kienyeji (olukina), kutafuta kuni na kuchota maji mtoni. Mambo haya yalimpatia msingi imara kabisa kwa shughuli za maisha yake ya usoni.
Alijiunga na Shule ya Msingi ya Nambale mwaka 1946 na kufanya mtihani wa ‘common entrance’ mwaka 1952 na akaendelea Shule ya Nambale Intermediate hapo mwaka 1953 alikofanya mtuhani wa Kenya African Preliminary Examination (KAPE) mwaka 1956 na akapita vyema. Kwa kuwa alitoka familia isiyokuwa na uwezo mkubwa, aliona hafadhali asiendelee na elimu ya juu na akatafuta riziki ili aweze kuwasaidia wazazi na ndugu zake. Nafasi ya kwanza aliyopata kuhusiana na utaalamu wake ilikuwa ni MedicalTraining School ya Kisumu mapema mwaka 1957, lakini baadaye aliwacha mafunzo hapo na kujiunga na Railway Training School huko Jinja alikopata mafunzo ya ukarani (clerk). Baada ya mafunzo ya miezi sita alipewa kazi huko Tororo Railway Station katikati ya mwaka 1957 ambako alifanya kazi kwa mda mfupi kabla kupelekwa kufanya kazi Kampala Railway Station. Alifanya kazi hapo hadi mapema mwaka 1959 alipopelekwa Railway Training School (RTS) Nairobi alipopata mafunzo ya Naibu wa Mkuu wa Stesheni (Assistant Station Master) kwa miezi sita na baadaye alipelekwa Kiu Railway Station. Baada ya hapo alifanya kazi katika stesheni mbalimbali ikiwa ni pamoja na Fort Hall Murang’a, Simba, Lukenya, Sultan Hamud, Embakasi, na Dagorreti. Baada ya hapo alirudi RTS akapate mafunzo zaidi awe Mkuu wa Stesheni (Station Master). Halafu akaendelea na kufanya kazi Eldoret Railway Station kama Msimamizi wa Stesheni (Station Foreman) katika mwisho wa miaka ya sitini hadi 1970 alipohamishwa na kwenda Nairobi Railway Station kama Yard Foreman kabla ya kuongezwa mamlaka na kupelekwa ofisi ya tikiti za upper class katika stesheni kuu (main station upper class booking office) kama msimamizi wa tikiti za reservations. Alifanya kazi katika ofisi hii hadi alipostaafu Shirika la Reli hapo 1992 baada ya miaka 35 ya kazi imara kabisa.
George Omoyi alikutana na kumuoa Faice Alice Mayabi (Namudu) ambaye kwa sasa ni ‘Mshemasi’ (Lay Canon) kanisani, hapo Machi 9, 1960 na baadaye akahalalisha ndoa yake mwaka 1979. Alibarikiwa kupata watoto watano, mmoja wa kike na wane wa kiume, wanaoitwa, Abigail, Samuel, Geoffrey, Vincent na Samson. Amewacha wajuku wake Ruth, Faith, John, Brigid, Elizabeth, Joy, Ashley, Imelda, Baby Joshua, Michelle na Aydan. Ndugu zake Peter, Morris, Janet, Maximilla, Hannington, Naliaka, Adhiambo, Nabwire, Patrick, Wandera, Narotso, Nekesa, Khadudu, Thomas na Barasa na mama wa kambo Nabwire. Alikuwa pia kakake marehemu Maloba Lukoba na Henry Lukoba. Alikuwa mkwe wa Lydia Makhandia Omoyi, Alice Kariuki, Lawrence Mugala Mugasiali, Florence Murema. Alikuwa mpwa wa Lambert Barasa, Ni babake mkubw Kenneth Kaunda Odulwa, Julius Okuku, Arthur Lukoba and Charles Lukoba wote wakazi New Jersey Na pia alikuwa mjomba wa Beatrice Maloba mkazi wa New York. Alikuwa binamu wa Abigail Lunzalu and Olivia Kunguru wakazi wa Texas.
Wakati wote alipokuwa akifanya kazi, George alituimia rasilimali zake kwa wingi sanakatika kuimarisha hali ya familia yake ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha ndugu zake na watoto, maswala ya ardhi na pia baadaye katika miradi yakuchuma pesa. Baada ya kustaafu alikazana sana na shughuli za maendeleo ya jumuiya. Alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Nambale Business Community, Mwanachama wa Baraza la Magavana (Board of Governors) wa Kisoko Girls High School na Nambale Boys High School. Pia, alikuwa Mweka Hazina wa Nambale Constituency Development Fund (CDF). Kwa juhudi zake mwenywe, aliongoza kuanzishwa kwa Nasira RC Secondary School na akiwa Mwenyekiti wa kwanza wa BOG na baadaye akahudumu kama memba. Aliongoza ujenzi wa barabara ya Nambale Bugeng’i kupitia Soko ya Nasira, pamoja na mradi wa umeme kutoka kona ya Tanga hadi Nasira. Alikuwa pia katika msitari wa mbele katika kuomba kubuniwa kwa Lokesheni ya Busibwabo iliyoundwa kutoka kwa Lokesheni ya Suo. Hadi alipoaga dunia, alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Baraza la Wazee wa Bukhayo (Bukhayo Council of Elders Association). Alianzisha ujenzi wa Hazanati ya Busibwabo. Alikuwa kiongozi mkuu (senior mentor) aliyehishimiwa sana na ukoo wake wabamenya wa Bukhayo.
George Omoyi alikuwa Mkristo wa dhati. Alikuwa mwanachama wa maisha wa Kenya Anglican Men’s Association. (KAMA). Alishughulika sana katika uanzilishaji na ujenzi wa kanisa la St Johns Buloma Church na alikuwa Mweka Hazina wa kanisa hilo. Wakati mmoja alihudumu kama mwanachama wa Baraza la Nambale Parokia na hata alipotuaga ghafla, alikuwa Mwenyekiti wa Fedha za Parokia hiyo. Daima alikuwa akipeana mawazo na maoni ya maana kuhusu maendeleo ya kanisa kwa jumla na alichangia kwa roho mkunjufu katika shughuli zake kwa kupeana rasilimali na hata wakati wake.
Mwenyenzi Mungu alimbariki George Omoyi na afya nzuri kwa mda mrefu maishani mwake. Julai 2007 alianza kulalamika kuwa kicha kilikuwa kinamuuma mara kwa mara na mbeleni alipata matibabu hapo Tanaka Nursing Home. Baadaye akasafiri hadiNairobi kwa matibabu zaidi ambako aligundulika kuwa na utomvu wa bongo (brain tumour) na ikabidi afanyiwe upasuaji wa haraka. Hapo Augusti 23, 2007, alifanyiwa upasuaji uliofanikiwa vyema an daktari alishauri apate matibabu zaidi kupitia radiotherapy na chemotherapy ambazo zilipendekezwa na kwa Daktari Kannan wa PJ Hinduja Hospital Mumbai huko India kati ya Oktoba na Novemba 2007. Alirudi nyumbani kuendelea kupata nafuu na kuendelea na matibabu. Wakati wote alipokuwa akipata matibabu, madaktari walikuwa wanasaidia sana familia na wakatutayarisha vyema kwa hali yoyote ile ingeweza kutokea. George alikazana sawasawa na akaendelea na matibabu yake bila kuchoka na hata hakukosa mara moja kufika kwa daktari na kupata madawa yake. Alipokuwa nyumbani kwao walikotoka wazazi wake huko Wilaya ya Busia hapo Ijumaa Januari 2, 2009 alimaliza chakula chake na akaelekea kupumzika kitandani na akalala makini kabisa hadi alipoamka asubuhi ya jumapili ndio ampe kwaheri mtoto wa kike na wajukuu wake waliokuwa wanaodoka kwa safiri ya kurudiNairobi, lakini hakuweza kula chochote siku nzima. Alipelekwa Tanaka Nursing Home apate usaidizi wa madktari na daktari alimshughulikia na akarudi nyumbani jioni. Lakini, hali yake iliharibika na ikaendelea kuzorota usiku wote. Mwishowe alituaga kwa amani hapo saa moja na dakika kumi na tano asubuhi siku ya Jumapili Januari 4, 2009. Kando yako walikuwa Mke wake, kakake Peter, mtoto wake Samson, na muuguzi wake Nicholas.
MWENYENZI MUNGU PEKEE ANAJUA
Mwenyenzi Mungu Pekee anajua vile uliishi maisha bora
Mwenyenzi Mungu Pekee anajua vile ulivyokuwa mme mwenye mapenzi
Mwenyenzi Mungu Pekee anajua vile ulivyokuwa baba mwenye kujali wanawe
Mwenyenzi Mungu Pekee anajua vile ulivyopenda ndugu zako
Mwenyenzi Mungu Pekee anajua vile ulivyoumia kwa maumivu
Mwenyenzi Mungu Pekee anajua vile ulivumilia maumivu bila kulalamika
Mwenyenzi Mungu Pekee anajua vile ulivyo mume shujaa
Mwenyenzi Mungu Pekee anajua vile ulivyo tulizwa roho na usalama
MWENYENZI MUNGU NDIYE HUPEANA NA MWENYENZI MUNGU NDIYE HUCHUKUWA
“Uliishi Maisha Kamilifu, Ulidumisha Imani na Mwenyenzi Mungu, na Mungu aiweke roho yako mahala pema peponi, Ameni!!!”